Trump akosolewa mdahalo wa Republican

Wagombea wa Republican waWagombea urais wa chama cha Republican nchini Marekani wamejibizana kuhusu njia bora zaidi za kudumisha usalama wa taifa na kukabiliana na Islamic State (IS) kwenye mdahalo wa kwanza tangu kutokea kwa mashambulio ya California na Paris. Mgawanyiko mkubwa umetokea kati ya wale wanaotetea kuwepo kwa upeelezi zaidi na wale wanaotetea haki za kiraia.
Mgombea anayeongoza, Donald Trump, amelazimika kujitetea kutokana na pendekezo lake kwamba Waislamu wazuiwe kuingia Marekani.
Mgombea mmoja anayempinga vikali, Jeb Bush, amemwita “mgombea wa vurugu”.
Seneta Marco Rubio na Ted Cruz pia wametofautiana kuhusu juhudi za serikali kupeleleza raia wake.
“Hatuzungumzi kuhusu kutengwa kwa watu, tunazungumzia usalama,” amejitetea Bw Trump. “Hatuzungumzi kuhusu dini, tunazungumza kuhusu usalama.”
Mjadala huo upesi ulipanuka na kuanza kukumbatia masuala pana kama vile sera ya kigeni na usalama wa kitaifa.
Pendekezo jingine la Trump, la kufunga mtandao wa intaneti kuzuia IS kuandikisha wanachama, umejadiliwa sana huku mfanyabiashara huyo tajiri akizomewa alipojaribu kujitetea.
Bw Trump ameonekana kukanganyikiwa na hisia za umati, akisema: “hawa ni watu wanaotaka kutuua jameni.”

Comments