Mapya yaibuka kashfa mabilioni ya uingereza
Kashfa ya ufisadi kwenye mauzo ya hati fungani za Dola 600 (sawa na Sh. trilioni 1.3) ambazo Serikali ya Tanzania iliziuza kwa Benki ya Standard ya Uingereza mwaka 2012 imeingia sura mpya baada ya taasisi isiyo ya kiserikali ya Kupambana na Rushwa ya Uingereza (Corruption Watch), kutaka wahusika wa sakata hilo washitakiwe mahakamani.
Kwa mujibu wa taarifa ya Corruption Watch iliyotolewa na Nipashe kupata nakala yake jana, ilipinga kitendo cha watuhumiwa wa suala hilo kuachwa kufuatia uamuzi wa makubaliano ya mahakamani (DPA) kati ya Taasisi ya Kupambana na Rushwa Kubwa ya Uingereza (SFO) na Benki ya Standard Novemba 30, mwaka huu.
Mahakama ya Crown Court Southwark ya jijini London, Uingereza, Novemba 30, mwaka huu iliamuru Serikali ya Tanzania irejeshewe Dola za Marekani milioni sita (sawa na Sh. bilioni 12.6) kutokana na kubainika kuwapo kwa udanganyifu baada ya kesi hiyo kufunguliwa kwenye mahakama ya kwamba asilimia moja ya mkopo huo ambayo ni Dola milioni sita zililipwa kwa Kampuni ya EGMA.
Hivi karibuni Nipashe liliripoti suala hili na kuwahusisha kwenye sakata hilo aliyekuwa Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya kama mmiliki wa Kampuni ya EGMA, Ofisa Mkuu Mtendaji wa zamani wa Benki ya Stanbic wa tawi la Tanzania, Bashir Awale, aliyekuwa Mkuu wa Uwekezaji wa benki hiyo, Shose Sinare, baadhi ya vigogo wa Serikali ya Tanzania na maofisa wa Benki ya Standard ya Uingereza.
Corruption Watch imesema kuwa makubaliano kati ya SFO na Benki ya Standard yalikuwa na mapungufu mengi kiasi cha kuiumiza Tanzania.
Kashfa yenyewe ilitokana na kitendo Benki ya Standard kukubali kuipokesha Serikali ya Tanzania kiasi cha Dola milioni 600 (Sh trilioni 1.3) mwaka 2012 kwa masharti ya kulipwa riba ya asilimia 1.4, lakini Benki ya Stanbic, tawi la Tanzania iliongeza asilimia moja na hivyo kufanya serikali kutakiwa kulipa riba ya asilimia 2.4.
Benki ya Stanbic ambayo ni tawi la Standard iliyokuwa ikishughulikia suala hilo ikishirikiana na maofisa wa Serikali ya Tanzania, ilidai nyongeza hiyo ilikuwa ni kwa ajili ya malipo kwa wakala yaani Kampuni ya EGMA iliyopewa kazi ya kushauri mauzo hayo ya hati fungani ingawa zilitumika kuhonga maofisa wa serikali.
Benki ya Standard ililazimika kuingia makubaliano na SFO baada ya kukiri kutoa rushwa kwa maofisa wa Tanzania, kwani makubaliano kama hayo ya DPA hutoa mwanya kwa kampuni zenye makosa kutoa fidia badala ya kuadhibiwa na Mahakama za Uingereza pale zinapokiri makosa na hasa yale yanayohusiana na rushwa na ufisadi.
Corruption Watch imedai kuwa Tanzania haikutendewa haki kwenye makubaliano kati ya SFO na Benki ya Standard kutokana na wahusika wa tuhuma hizo kutoshitakiwa.
Pia imeeleza kuwa makubaliano ya mahakamani yameipunja Tanzania iliyoambulia kiasi cha Dola milioni sita tu (sawa na Sh. bilioni 12.6), wakati haki ingetendeka ingepata kitita cha fedha kinachofikia kiasi cha Dola milioni 80 (sawa na Sh. bilioni 168).
Mambo manne yaliyoibuliwa na Corruption Watch.
Watuhumiwa kutoshitakiwa
Taasisi ya Corruption Watch imesema kuwa imeshangazwa na kutochukuliwa hatua zozote dhidi ya wahusika yaani maofisa wa Benki ya Standard au wale wa Stanbic wa tawi la Tanzania.
Kwa upande wa Tanzania, watu wanaotajwa kuhusika kwa mujibu wa hukumu ya Jaji Levetson wa Uingereza ni pamoja na Kitilya, ambaye kama mmoja wa wamiliki wa Kampuni ya EGMA, Awale na Sinare.
Pia maofisa waliohusika na sakata hilo kwa mfano Awale na Sinare, waliacha kazi katika benki ya Stanbic bila kuchukuliwa hatua.
Katika hukumu hiyo, Jaji Lord Levetson alisema wazi kuwa Sinare aliwaambia maofisa wa SFO kwamba alisikia bosi wake, Awale akizungumza kwa simu na Ofisa wa ngazi ya juu wa Benki ya Standard juu ya uhalali wa nyongeza ya riba kwa madai ilikuwa fedha kwa ajili ya kuwalainisha maofisa wa Serikali wa Tanzania na lilikuwa jambo la kawaida kwa nchi za Afrika.
Pia Corruption Watch walitaka maofisa wa Benki ya Standard waadhibiwe kutokana na kuidhinisha malipo kwa ajili ya rushwa wakati ni kinyume cha Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Uingereza.
SFO kutohoji wafanyakazi wa Stanbic
Corruption Watch pia wameponda hatua ya SFO ya kutegemea taarifa ya uchunguzi wa Benki ya Standatrd wakati wakifuatilia suala hilo.
Taasisi huyo ilisema katika taarifa yake ilikuwa kosa kwa SFO kutegemea taarifa ya maofisa wa Standard wakati walikuwa watuhumiwa wa kesi ile.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa SFO ilitakiwa kufanya uchunguzi wa kina wa jambo hilo kwani ulikuwa unahusisha masuala ya rushwa na ufisadi, ambayo ni makosa makubwa nchini Uingereza.
Corruption walishangazwa na hatua ya SFO kutofanya upelelezi wao nchini Tanzania ambako ndiko vitendo vya rushwa vilifanyika.
“Inashangaza kuona SFO hawakujishughulisha kwenda Tanzania na kuhoji wafanyakazi wa Benki ya Stanbic, ambao ndiyo walifichua habari ya ufisadi huu,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Corruption Watch inaamini kuwa laiti SFO ingehoji wafanyakazi wa Stanbic, basi ingefahamu watu waliopokea rushwa kupitia benki hiyo kutokana na kashfa hiyo.
Mpango ulipingwa na IMF
Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lilipinga mpango wa Serikali ya Tanzania kuuza hati fungani kwa kiasi hicho cha Sh. trilioni moja kwa madai ilikuwa hasara kwa Tanzania.
Pia Shirika la Habari la Uingereza (Reuters), lilimkariri ofisa mmoja wa benki akidai kuwa mpango huo ulikuwa maafa kwa Tanzania Machi, 2012.
Corruption Watch imesema kuwa Tanzania ilitakiwa kulipwa mara 10 zaidi kama Dola milioni 80 badala ya Dola milioni sita.
“SFO ilitakiwa kuzingatia hilo wakati ikichunguza juu ya kashfa hiyo ili kupata ukweli kamili juu ya suala hilo na athari zake kiuchumi na hasa kwa Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Taasisi hiyo ilisema kuwa kwenye makubaliano kati ya SFO na Standard, yalitakiwa yawe kwa faida ya jamii.
“Pia makubaliano yale yalitakuwa kuzingatia hasara iliyopata Serikali ya Tanzania ili ipate mgawo mkubwa kutokana na uamuzi ule,” iliongeza taarifa hiyo.
Benki ya Standard ilitakiwa kupewa adhabu kubwa
Corruption Watch imesema kuwa SFO ilikosea kuingia makubaliano na Benki ya Standard kwa misingi wao ndiyo waliripoti juu ya kuwapo kwa rushwa kwenye dili lake na Serikali ya Tanzania.
Taasisi ilisema kuwa suala hilo lilifichuliwa na wafanyakazi wanne wa Benki wa Stanbic wa tawi la Tanzania na siyo Benki ya Standard ambayo ilitakiwa kupewa adhabu kubwa zaidi.
“Hawa wafanyakazi wanne walieleza kuwa kuna fedha zilikuwa zimetolewa kwenye benki hiyo katika mazingira ya kutatanisha na kulipwa kwa maofisa wa Kampuni ya EGMA katika siku tisa,” ilisema taarifa ya Corruption Watch.
Taasisi hiyo ilisisitiza kuwa kama SFO wangekuwa makini, wangepata taarifa juu ya suala hilo kwani wafanyakazi wa Stanbic walisharipoti suala hilo Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Pia Corruption Watch ilisema rushwa ile ilifanya dili hiyo ya mabilioni kukosa ushindani kwani mabenki mengine yalikosa fursa hiyo kutokana na kutotoa rushwa
Comments
Post a Comment