Tiger Woods kurejea uwanjani

Mwanamichezo nguli aliyewahi kuwa mcheza golf namba moja duniani Tiger Woods, amesema kwamba ana matarajio ya kushinda michuano mikubwa zaidi katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Woods, ambaye mwishoni mwa mwezi huu atatimiza umri wa miaka 40, amedondokea katika nafasi ya 414 katika viwango vya ubora wa mchezo wa golf duniani na alishinda taji lake la 14 kwa mara ya mwisho mnamo mwaka 2008.
Tiger aliwahi kufanyiwa upasuaji wa mgongo mwezi September mwaka huu hiyo ikiwa ni mara ya pili katika kipindi cha miezi 18 lakini ana matarajio ya kucheza kwa ufanisi zaidi mwanzoni mwa mwaka mpya wa 2016.
"Najiona wapi binafsi katika kipindi cha miaka mitano ama kumi ijayo? Alinukuliwa Tiger akisema na kuongeza kwamba bado ninao uwezo wa kucheza golf katika kiwango cha ubora wa hali ya juu na kushinda katika michuano mikubwa na kutwaa tuzo" na haya aliyaandika katika tovuti yake binafsi pia.
Woods amejiwekea rekodi ya kushinda katika mchezo wa golfu kwa wiki mia sita themanini na tatu kama bingwa wa dunia katika mchezo huo lakini alipoulizwa kuwa anaingia katika muongo wa tano akiwa na umri mkubwa , Tiger alijibu suala hilo kwa kusema kwamba "kiakili watu wanaonifahamu, wananijua kama kijana mdogo mwenye miaka mitano".

Comments