Mourhino afutwa kazi chelsea rasmi

Meneja wa klabu ya Chelsea ya Uingereza amefutwa kazi baada ya klabu hiyo kuandikisha msururu wa matokeo mabaya.
The Blues walishinda Ligi ya Premia msimu uliopita lakini msimu huu mambo yamekuwa kinyume, na wamo alama moja tu juu ya eneo la kushushwa daraja ligini.
Bodi ya klabu hiyo ilikutana jana kujadili hatima ya Mourinho chini ya mmiliki wa klabu hiyo, Mrusi Roman Abramovich.
Klabu hiyo kupitia taarifa imesema mkataba kati ya klabu na meneja hiyo umekatishwa kwa maelewano kati ya pande zote mbili na ikamtakia kila la kheri Mourinho.
“Sifa zake Stamfrod Bridge na Uingereza zinajieleza na daima anakaribishwa kurejea Stamford Bridge,” klabu hiyo imesema kupitia taarifa.
“Sasa tutaangazia kuhakikisha kikosi chetu kilichojaa wachezaji wenye vipaji kinafikia uwezo wake. Hakutakuwa na taarifa zozote zaidi kutoka kwa klabu hadi kocha mpya ateuliwe.”
Mreno huyo mwenye umri wa miaka 52 amekuwa Chelsea kwa kipindi cha pili, kilichoanza Juni 2013.
Chelsea walimaliza alama nane mbele kileleni msimu uliopita na kutwaa taji pamoja na Kombe la Ligi lakini mwaka huu wameanza vibaya, wakishindwa mechi tisa kati ya 16 ligini kufikia sasa.
Mechi ya mwisho kwa Mourinho kwenye usukani ilikuwa Jumatatu walipochapwa na viongozi wa ligi Leicester City 2-1.
Mourinho alitia saini mkataba mpya wa miaka minne tarehe 7 Agosti mwaka huu na ndiye meneja aliyefanikiwa zaidi akiwa na Chelsea.
Alishinda mataji matatu ya Ligi ya Premia kipindi chake cha kwanza katika klabu hiyo kati ya 2004 na 2007.
Pep Guardiola, Guus Hiddink, Brendan Rodgers na Juande Ramos na miongoni mwa wanaopigiwa upatu kumrithi.

Comments

Popular posts from this blog

LOWASA KUZUNGUKA TANZANIA NZIMA KUWASHUKURU WA TATANZANIA KWA KUMPIGIA KURA

Mapya yaibuka kashfa mabilioni ya uingereza

MELI YA MV ROYAL YAWAKA MOTO BAHARI YA HINDI